FAIDA YA NGUVU ZILIZOMFUFUA YESU
Bwana Yesu asifiwe milele!
Faida nyingine unayotakiwa kunufaika nayo unapokuwa unazo ndani yako, nguvu zilizomfufua Yesu ni hii: *“Imani uliyonayo kwa Mungu, katika Yesu Kristo, na katika neno lake – inapata uhai na inakuwa na uwezo wa kuzaa”!*
Hii ni kwa sababu biblia inasema “tena kama Kristo hakufufuka, basi, kuhubiri kwetu ni bure na Imani yenu ni bure” (1 Wakorintho 15:14). Hebu oanisha maneno ya mstari huu na maneno ya mistari hii: “Imani isipokuwa na matendo, imekufa nafsini mwake” (Yakobo 2:17).
“Lakini wataka kujua, wewe mwanadamu usiye kitu, kwamba imani pasipo matendo haizai?” (Yakobo 2:20). “Maana kama vile mwili pasipo roho umekufa, vivyo hivyo na imani pasipo matendo imekufa” (Yakobo 2:26).
Imani uliyonayo kwa Mungu katika Kristo, na katika neno lake inatakiwa iwe hai! Imani yako hiyo isipokuwa hai ndani yako ni bure…yaani inakuwa haina faida kwako, wala msaada wowote kwako! Ina maana ni imani usiyoweza kuitumia! …kwa kuwa imekufa na haina uhai nafsini mwake!
Kwa mfano: Kufuatana na Warumi 10:9, 10 ukiamini au ukiwa na imani moyoni mwako, unatakiwa uokoke. Wokovu unazaliwa kama tunda mojawapo la imani iliyo ndani yako! Pia tunajua ya kuwa; “mashetani nao waamini na kutetemeka” (Yakobo 2:19), lakini hakuna shetani aliyewahi – kuokoka kwa Imani hiyo? Na pia, tuna wanadamu wanaoamini ya kuwa Mungu yuko, lakini hawakubali kuokoka! Hii ina maana ya kuwa unaweza ukawa na imani na isikusaidie.
Kwa nini? Kwa sababu; 1. Imani pasipo matendo imekufa; na 2: Imani pasipo matendo haizai! Je, Imani uliyonayo iko hai au imekufa? Je, Imani uliyo nayo ni tasa au inauwezo wa kuzaa kilichomo ndani yake? Kumbuka – hata ikiwa imani yako uliyonayo katika Kristo Yesu na katika neno lake inapigwa vita (1 Timotheo 6:12) au inajaribiwa (Yakobo 1:3) – bado imani hiyo inatakiwa ikuzalie matunda mazuri!
Ndiyo maana imeandikwa hivi: “Ndugu zangu, hesabuni ya kuwa ni furaha tupu, mkiangukia katika majaribu mbalimbali mkifahamu ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi (uvumilivu). Saburi na iwe na kazi kamilifu, mpate kuwa wakamilifu na watimilifu bila kupungukiwa na neno” (Yakobo 1:2-4).
Ni maombi yetu kwa ajili yako wiki hii ya kwamba: Nguvu zilizomfufua Yesu zilizomo ndani yako, zitaihuisha imani yako, ili iwe hai – kama imekufa! Na kama iko hai – basi, iendelee kuwa hai na izae matunda ya kile kilichobebwa na imani hiyo! …Katika jina la Yesu – Amen!
Comments
Post a Comment