1.FAIDA YA NGUVU ZILIZOMFUMFUA YESU
Hili ni somo lililofundishwa Na Mwl Mwakasege nakuletea ujifunze kitu naanza Na sehemu ya kwanza
Bwana Yesu asifiwe milele!
Je umeokoka? Ikiwa umeokoka, ujue basi ya kuwa, nguvu za Mungu zilizomfufua Kristo toka kwa wafu, zimo ndani yako! Nguvu hizi zimebebwa na Roho Mtakatifu aliye ndani yako! Hii ni kwa sababu imeandikwa hivi “lakini ikiwa Roho yake yeye aliyemfufua Yesu katika wafu anakaa ndani yenu yeye aliyemfufua Kristo Yesu katika wafu ataihuisha na miili yenu iliyo katika hali ya kufa, kwa Roho wake anayekaa ndani yenu” (Warumi 8:11).
Je, unajua faida kwa ajili yako – sasa wakati huu – yaani katika ulimwengu huu, kwa nguvu za Mungu zilizomfufua Kristo kukaa ndani yako? Na kama unazijua – je; unazitumia na kufaidika kwa kiwango kipi katika maisha yako? Hebu tafakari faida chache zifuatazo:
*Faida 1: Nguvu zilizomfufua Yesu zilizomo ndani yako zinakupa uwezo wa kukusaidia kubadili mfumo na kiwango chako cha kufikiri!...*
ili uwe na mawazo yaliyo bora kuliko ya wale wanaokuzunguka! Biblia inasema: “Basi mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo…yafikirini yaliyo juu…mkivaa utu mpya, unaofanywa upya upate ufahamu sawasawa na mfano wake yeye aliyeuumba” (Wakolosai 3:1, 2,10). Nguvu zilizomfufua Yesu zinakupa nafasi ya kuweza kujua “mawazo” ya Mungu juu ya mambo yanayokuhusu (Isaya 55:8,9 na Yeremia 29:11) – ili katika mawazo hayo ya ki – Mungu uweze kujenga mfumo wako wa maisha, na wa utendaji wako wa kazi (Mithali 23:7a)!
Jizoeze kutumia nguvu zilizomfufua Yesu zilizomo ndani yako kupambana na kuondoa “mawazo” ndani yako, yanayozuia au yanayokandamiza, kiwango cha mafanikio yako, kisifikie kiwango kile alichokikusudia Mungu kwa ajili yako! “Maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili; (maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome) tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; na tukiteka nyara kila fikira ipate kumtii Kristo”.
Uwezo huu wa Mungu umo ndani yako! Ni uwezo unaoweza kubadili kufikiri kwako, kwa kiasi cha kukupa kuwaza na kufahamu mambo kama Mungu atakavyo! Je, unatumia na kuufaidi uwezo huu kwa kiwango gani?
Tunakuombea ili kiwango chako cha kufaidika na nguvu zilizomfufua Yesu zilizomo ndani yako kiongezeke, na uone matokeo yake katika maisha yako!
nitakuletea faida ya 2.
Mbarikiwe!!
Comments
Post a Comment